Uongozi wa klabu ya Ruvu Shooting kupitia kwa msemaji wake Masau Bwire
umemuomba radhi mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi kufuatia kufanyiwa
tukio lisilo la kiungwana na mchezaji wao Mau Bofu.
Masau Bwire amesema wao kama uongozi wa Ruvu Shooting, pamoja na
mchezaji mwenyewe wamekiri kufanya kosa hilo na wanamuomba radhi Okwi
mwenyewe, uongozi wa Simba pamoja na wapenda soka wote.
Bofu alimpiga kiwiko Okwi katika dakika ya 43 ya mchezo kati ya timu
hizo siku ya Jumapili wikiendi iliyopita, kwenye Uwanja wa Uhuru, ambapo
mwamuzi alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja licha ya kuwa
tayari alikuwa na kadi ya njano.
Kitendo hicho kilisababisha Okwi asiendelee na mchezo hivyo
kulazimika kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo. Katika
mchezo huo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Okwi anaongoza orodha ya wafungaji msimu huu akiwa na mabao 12 hadi
sasa, wakati klabu yake ya Simba ikiwa kileleni mwa msimamo ikiwa na
alama 38.

0 comments :
Post a Comment