OKWI AREJEA SIMBA SC KUCHEZA KWA MUDA WAKATI KESI YAKE NA YANGA IKIENDELEA MWENYEWE ASEMA ANALINDA KIPAJI CHAKE



STAILI ile ile waliyotumia Yanga SC kumpata mshambuliaji Emmanuel
Arnold Okwi ndiyo ambayo klabu yake ya zamani, Simba SC inaitumia kumrejesha
kundini Mganda huyo.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari jioni ya janaa mjini Dar es Salaam, Okwi amesema
kwamba amesaini Simba SC mkataba huru wa muda, baada ya Yanga SC kumpa barua ya
kusitisha mkataba naye jana pamoja na kumshitaki Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF).


Okwi amesema ameamua kuomba kuichezea Simba SC kipindi hiki ambacho ana
matatizo na Yanga SC ili kulinda kipaji chake, kwa kuwa hata FIFA haitaki
mchezaji akae bila kucheza.
 

“Sasa wakati Yanga wanaendelea na kesi yao, mimi ninaomba nichezee Simba
SC ili kulinda kipaji changu. Nimewaandikia barua TFF na FIFA pia na nina
matumaini usajili wangu utaidhinishwa, kwa sababu mimi si tatizo katika
hili,”amesema.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans
Poppe amesema kwamba wamemsaini mchezaji huyo baada ya kupitia kwa kina suala
lake na Yanga SC na kugundua haki ipo upande wa mchezaji.

“Baada ya kulipitia suala lake na Yanga kwa undani kabisa na vielelezo ambavyo
mchezaji mwenyewe ametupatia, tumejiridhisha tuko sahihi kumsaini ili acheze
mpira kunusuru kipaji chake kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga
SC,”amesema Poppe.
 

Tayari Simba SC imetuma jina la mchezaji huyo katika usajili wake TFF na
ataungana na Mganda mwenzake, Joseph Owino, Warundi Pierre Kwizera na Amisi Tambwe
na Mkenya, Paul Kiongera katika wachezaji watano wa kigeni.


“Tumewaandikia barua TFF kuomba kumtumia mchezaji huyu kwa muda wakati kesi
yake na Yanga inaendelea, tumeambatanisha na barua yake ambayo yeye anatuomba
kucheza kwetu kulinda kipaji chake,”amesema Poppe.

 
    -Okwi akiwa ameshika jezi yake nbamba 25 kwa pamoja na HansPoppe


Okwi aliichezea Simba SC tangu mwaka 2009 kabla ya Januari mwaka jana
kuuzwa kwa dola za Kimarekani 300,000 Etoile du Sahel ya Tunisia.


Etoilehaikulipa fedha hizo Simba SC na baadaye ikaingia kwenye mgogoro na Okwi,
aliyedai hakulipwa pia mishahara yake kwa miezi mitatu. Okwi akawafungulia
Etoile kesi FIFA na akaomba wakati mgogoro wao unaendelea, aruhusiwe kuchezea
timu yoyote kulinda kipaji chake, ndipo akajiunga na SC Villa ya kwao.

Akiwa SC Villa ndipo aliposaini Yanga SC Desemba mwaka jana na pamoja na
mapingamizi yaliyoanzia ndani, na baadaye klabu yake, Etoile- lakini Okwi
aliidhinishwa kuichezea timu hiyo ya Jangwani.

Okwi aliichezea Yanga SC mechi 11 na kuifungia mabao matano lakini kuelekea
mechi tano za mwisho za Ligi Kuu msimu uliopita akaingia kwenye mgogoro na
klabu hiyo. Okwi alisusa kushinikiza amaliziwe fedha zake za usajili na
mgogoro wao umeendelea huku mchezaji huyo akiwa amesusa tangu Machi, miezi
minne tu baadaye tangu asajiliwe.

Vikao kadhaa vimekwishafanyika baina ya Okwi na Yanga SC tangu hapo kutafuta
suluhu ya suala hilo na kikao cha mwisho leo baina ya mchezo huyo na Mwenyekiti
wa klabu hiyo, Yussuf Manji matokeo yake ni nyota huyo kurejea Msimbazi.

Kuhusu deni lao la dola 300,000 kumuuza mchezaji huyo Etoile, Poppe amesema
haihusiani kabisa na usajili wake huu wa sasa. “Ile kesi yetu ya madai ya fedha
zetu kule FIFA ilikwishamalizika na vielelezo vyote vilipelekwa, bado kutolewa
hukumu tu,” amesema. 









Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment