Mchezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Ally Samatta akiwa na klabu
yake ya KRC Genk amefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Ubelgiji baada
ya kushinda mchezo wa nusu fainali dhidi ya Kortrijk.
Katika mchezo huo uliopigwa usiku wa kuamkia leo Samatta amecheza
dakika zote 90 na kuisaidia timu yake kushinda bao 1-0 katika nusu
fainali ya pili hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3 na Genk kufuzu
kwa faida ya goli la ugenini baada ya Genk kupoteza 3-2 kwenye nusu
fainali ya kwanza.
Bao pekee la Genk limefungwa na kiungo Ibrahima Seck ambaye ni raia
wa Senegali katika dakika ya 15 akimalizia pasi ya Mhispania Alejandro
Pozuelo Melero.
Katika mchezo wa fainali, Genk inasubiri kujua mpinzani wake ambaye
atashinda kwenye nusu fainali ya pili kesho kati ya timu za Club Brugge
na Standard Liege. Matokeo katika mchezo wa kwanza Liege wanaongoza kwa
mabao 4-1.
Samatta jana amecheza mechi yake ya nne tangu apone majeraha ya goti
yaliyomweka nje kwa miezi kadhaa. Nahodha huyo wa Taifa Stars pia
amefikisha michezo 74 ndani ya klabu hiyo ambayo alijiunga nayo Januari
2016.


0 comments :
Post a Comment