TIMU
ya Azam FC imerudi katika nafasi ya pili baada ya kuichapa Ndanda FC ya
Mtwara 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara usiku wa
leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Azam
FC inafikisha pointi 33 baada ya mechi 16 za Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL), ikizidiwa pointi mbili na vinara Simba SC, ambao
kesho wanacheza mechi yao ya 16 dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Shukrani kwa mabao matatu ya nguvu yaliyofungwa na washambuliaji Yahya Zayed, Shaaban Idd na winga Enock Atta, yaliyoizamisha kabisa Ndanda, ambayo ilionyesha upinzani mkali katika mchezo huo.
Iliwachukua
dakika ya 25 Azam FC kuweza kupata bao la uongozi, likifungwa na Zayd
alipokea pasi safi ya Shaaban na kuwatoka mabeki wa Ndanda kabla ya
kupiga shuti zuri nje kidogo ya eneo la 18 lililotinga wavuni.
Dakika tano baadaye Azam FC ilinufaika kwa mpira wa adhabu ndogo, baada ya winga Enock Atta kuitumia vema na kufunga bao la pili kwa mpira wa moja kwa moja uliomshinda kipa wa Ndanda, Jeremiah Kisubi.
Ndanda ilirejea mchezoni na kujipatia bao lake pekee lililofungwa na Nassor Kapama, kwa mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo uliomshinda kipa wa Azam FC, Razak Abalora na kufanya mpira huo uende mapumziko kwa wenyeji hao kuogoza 2-1.
Azam FC ilihitimisha ushindi wake kipindi cha pili baada ya Shaaban kuipatia bao la tatu akifunga kiustadi akiunganisha pasi safi ya juu ya winga Idd Kipagwile, ambaye naye alikuwa kwenye kiwango kizuri.
Katika mchezo huo, Azam FC ilimkosa Kocha wake Mkuu, Aristica Cioaba, ambaye alikuwa jukwaani baada ya kufungiwa na Bodi ya Ligi (TPLB) wakidai alionyesha ishara mbaya kwa mashabiki kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga.
Huu ni mwendelezo wa Bodi hiyo kuendelea kumsakama kocha huyo bila ushahidi dhahiri, ambapo hii ni mara ya pili inamfungia, kifungo cha awali wakimuhusisha ametoa lugha chafu kwa waamuzi wakati wa mchezo wa Azam FC dhidi ya Ruvu Shooting.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea kuwepo kambini kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Simba utakaofanyika Uwanja wa Taifa Jumatano ijayo saa 10.00 jioni, ambapo kesho Jumapili itaanza programu kujiandaa na mechi hiyo.

0 comments :
Post a Comment