>>VIINGILIO 5,000/= HADI 30,000/=
Release No. 019
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 1, 2013
KUONA TAIFA STARS, CAMEROON 5,000/-
Kiingilio cha chini kwenye mechi ya FIFA
Date kati ya Taifa Stars na Cameroon itakayochezwa Jumatano (Februari 6
mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa ni sh. 5,000 kwa
viti vya kijani.
Viti vya bluu ni sh. 7,000 wakati viti
vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000. Kwa viti vya VIP viingilio ni
kama ifuatavyo; VIP C sh. 15,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A sh. 30,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla
ya mchezo katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni
Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohia/Samora, kituo cha mafuta
OilCom Ubungo, Dar Live Mbagala na kituo cha mafuta Buguruni.
FECAFOOT YATAJA NYOTA WAKE 21, ETO’O NDANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Cameroon
(FECAFOOT) limetaja msafara wake wa watu 36 wakiwemo wachezaji 21 wa
timu yao ya Taifa Indomitable Lions) wakiongozwa na nahodha Samuel Et’oo
Fils kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumatano.
Kiongozi wa msafara wa timu hiyo
itakayoanza kuingia nchini keshokutwa (Februari 3 mwaka huu) ni
Mwakilishi wa Serikali ya Cameroon, Dieudone Wassi. Naibu kiongozi wa
msafara wa Cameroon itakayofikia hoteli ya New Africa ni Makamu wa Rais
wa FECAFOOT, John Ndeh.
Mbali ya Et’oo, wachezaji wengine
waliomo kwenye msafara huo ni Charles Itandje, Benoit Assou Ekoto, Jehu
Rustand Youthe (Union Douala), Fabrice Olinga Essono, Allam Nyam, Bouba
Aminou, Benoit Angwa, Herve Tchami, Henri Bedimo, Nicolas Nkoulou, Jean
Makoun, Jean Kana Biyick, Joel Matip, Vincent Aboubakar, Alexandre Song,
landre Nguemo, Pierre Wome, Jean Nyontcha, Achille Emana na Charles
Eloundou.
Wengine ni Andre Nguidljol Nlend
(Mkurugenzi wa Utawala FECAFOOT), Jean Paul Akono (Kocha Mkuu), Martin
Ndtouungou Mpile (Kocha Msaidizi), Jacque Songo’O (Kocha wa makipa), Dk.
Baoubakary Sidiki (Daktari wa Timu) na Emmanuel Francis Ambane
(Psychologist).
Pia wapo Tchonkontey Monkam (Fitness
Trainer), Rigobert Song (Meneja wa Timu), Aoudou Mvotoung (Team
Security), Fouda pascal Linus (Ofisa Habari FECAFOOT), Boubakar Ndou
(Meneja Vifaa), Daniel Tcheuffa Tecky (Physiotherapist), Elias Kalaguem
(Physiotherapist) na Justin Addo (Wakala wa Mechi).
Wakati huo huo, kikosi cha Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kitaingia kambini kesho
jioni (Februari 2 mwaka huu) kwenye hoteli ya Tansoma.
YANGA, MTIBWA SUGAR KAZI KWELIKWELI
Yanga na Mtibwa Sugar zinapambana kesho
(Februari 2 mwaka huu) katika moja ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha ndiye
atakayechezesha mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali, kwani
wakati Yanga ikiongoza ligi hiyo, wapinzani wao Mtibwa Sugar katika
mechi iliyopita walilala mbele ya Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho
katika msimamo wa ligi kwa sasa.
Polisi Morogoro itakuwa mwenyeji wa
African Lyon kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro wakati Uwanja wa
Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo
Shooting na Ruvu Shooting inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa.
Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi
mbili. Simba itaumana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
huku Tanzania Prisons ikiikabili Coastal Union katika Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.
VILLA SQUAD, MORO UNITED UWANJANI FDL
Villa Squad na Moro United zinaumana
kesho (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja
ya mechi za kundi B za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza mzunguko
wa lala salama.
Kundi A litakuwa na mechi kati ya Mbeya
City na Burkina Faso itakayochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya,
Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, na Polisi
Iringa dhidi ya Mkamba Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora
mjini Iringa.
Mechi nyingine ya Kundi B itakuwa
Transit Camp na Ndanda itakayochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
Kundi C ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma),
Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto, Manyara), Polisi Mara na Pamba
(Uwanja wa Karume, Musoma), Polisi Tabora na Rhino Rangers (Uwanja wa
Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika
mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi wa kila kundi atapanda
daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments :
Post a Comment